KWA Ambakisye Mwakabenga (70), kuungua kwa soko la SIDO jijini Mbeya katikati ya mwezi huu wa Septemba, 2011 kumemuacha katika misiba miwili.Kwanza ni kumuacha katika lindi la umaskini mkubwa huku akiwa hana mbele wala nyuma kwani kibanda chake cha kuuza maziwa kilikuwa ni rasilimali pekee iliyokuwa inaendesha maisha yake, mkewe mwenye miaka 65 pamoja na wajukuu zao watatu. Lakini pia ni kumtia katika deni kubwa kwa sababu mali za karibu Sh400,000 zilizokuwa kibandani kwake zilitokana na mkopo wa fedha aliokuwa amechukua kwenye taasisi mbalimbali mjini Mbeya ili walau aweze kuendesha shughuli za uchumi. “Sina mtoto wa kunisaidia, watoto wangu wanne walikwishafariki na wakaniachia wajukuu 15. Baadhi wamekua wanajitegemea, lakini hapa ninao watatu ambao daima husubiri nihangaike hapa ili waweze kula. Sasa na umri huu mjukuu wangu nitakuwa mgeni wa nani?” analalamika Mzee Mwakabenga. Mwakabenga ni miongoni mwa wahanga zaidi ya 1,700 waliounguliwa mabanda ya biashara katika ajali hiyo ambayo thamani ya mali zilizoteketea bado haijajulikana. Hata hivyo, mzee huyo ambaye ameshindwa kujenga kibanda kingine kutokana na kukosa fedha, anaweza kukumbwa na tatizo la kuhamishwa sokoni hapo kufuatia kauli ya Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, aliyoitoa mara baada ya tukio hilo kwamba lazima wafanyabiashara wengine wapungue sokoni hapo na kubakia 969 tu kati ya wafanyabiashara 1,206 wanaotambulika na serikali.Uamuzi huo umepingwa na wengi ambao wanasema Serikali haiwatendei haki kwa kutoa uamuzi wa aina hiyo pamoja na kuwataka wajenge vibanda vya mbao badala ya matofali ambavyo walikwishaanza kuvijenga. Sofina Pera (48), fundi cherehani na mama wa watoto wanne, alisema kwamba ubabe wa serikali wa kuwalazimisha kujenga mabanda ya mbao utazidi kuwatia umaskini ikiwa moto mwingine utatokea. Aidha, alisema kwamba mpaka sasa hawajui nini cha kufanya kwa sababu wametumia gharama kubwa kununua tofali na mchanga na hawafahamu watapata wapi fedha nyingine za kununulia mbao. Mtaji unazidi kupotea pasi kuzalisha.Alisema alikuwa akiitegemea biashara yake ya kushona nguo katika kuendesha maisha ya kila siku ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wake wanne walioko shule. “Mimi pamoja na hawa wenzangu, hatuelewi nini tufanye kwa wakati huu maana tulikwisha kuchangishana fedha na tukanunua matofali yaliyoko hapa tayari kwa ujenzi, halafu tunaambiwa tusijenge; sasa hatuelewi fedha za kununulia tena mbao tutazitoa wapi,” alihoji Sofina. Alisema kwa sasa ubao mmoja unauzwa kati ya shilingi 8,000 na 10,000 ambapo kutokana na hali iliyopo sasa kuna uwezekano mkubwa wa bidhaa hiyo kupanda,hali ambayo wafanyabiashara wengi ambao walikwishanunua matofali watashindwa kujenga. Mfanyabiashara mwingine aliyeathirika na moto kuunguza soko, Jane Athanas anasema ameingia gharama mara mbili, ya kununua tofali, kujenga na kubomoa pamoja na kununua mbao, licha ya hasara waliyoipata kwa kuunguliwa na mali na mabanda yao. “Tumelazimika kubomoa vibanda baada ya serikali kutulazimisha tubomoe na tusijenge vibanda vya matofali kwa maelezo kwamba hili ni eneo la muda. Sisi tuko tayari kubomoa hata tukipewa miezi sita, lakini serikali haitusikilizi. “Tuliunguliwa na soko mwaka 2006 na kupata hasara, hakuna aliyetufidia, sasa safari hii tumeunguliwa tena, tunataka kujenga vibanda imara ambavyo walau vinaweza kuhimili moto tunaambiwa tusijenge. Hivi hawatuonei huruma?” alihoji Jane, ambaye anasema aliunguliwa na mali zenye thamani ya Sh40 milioni. Wiki iliyopita, Kandoro, aliwaamuru wafanyabiashara hao kutojenga vibanda vya kudumu kwa maelezo kwamba eneo hilo wamepewa kwa muda na SIDO na akawataka wale wote waliokwishajenga kuvibomoa mara moja. Tunajiuliza SIDO wenyewe wanasema ninik kuhusu kadhia ya wafanyabiashara hao ambao wengi wao wanauza bidhaa zinazotengenezwa na wajasiramali wanaosimamiwa na taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo. Naye Smart George alisema serikali ilipaswa kuwashirikisha kuhusu aina ya vifaa vya kujengea vibanda vipya na kusisitiza kuwa vibanda vya matofali vilikuwa salama zaidi na “ ndivyo vilivyosalimika katika matukio ya moto wa soko la Mwanjelwa mwaka 2006 na hata tukio la hapa SIDO”. “Serikali imetuingiza hasara kwa kushindwa kuzima moto kwa wakati, lakini pia haitendi haki kwa kutoa matamko ya ubabe,” Alisema George. Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo Charles Syonga, alisema wafanyabiashara hao wangependa kujenga kwa matofali kwa kuwa wamekwishapata fundisho kwa mara ya pili lakini kwa kuwa serikali imesema hawana budi kukubaliana na hali halisi. “Serikali ni serikali ikishasema kinachofuata ni utekelezaji, lakini kwa kweli tumechoshwa na kuunguliwa kila wakati, tungependa nasi tusikae kwa mashaka hata kama ni kwa muda mchache, tujenge vibanda vyetu kwa mkataba muda utakapofika tuhame,” alisisitiza Mwenyekiti. Akiongelea suala la baadhi ya wafanyabiashara kuhamishwa katika eneo hilo kupelekwa masoko mengine, alisema kuwa yeye kama kiongozi asingependa kwa kuwa kuhama kwao kutawafanya kuanza maisha upya kutokana na kupoteza wateja wao. Alisema pia kwamba, soko hilo lilikuwa likijihudumia lenyewe kwa huduma mbalimbali zikiwemo za ulinzi, maji na huduma muhimu, hivyo iwapo watu watapunguzwa italazimika kuchanga kiasi kikubwa cha fedha ili kukidhi matakwa hayo. Katika ziara fupi aliyoifanya Mkuu wa Mkoa akiongozana na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, aliwaagiza wafanyabiashara kusitisha kujenga vibanda kwa kutumia matofali kwa kuwa eneo hilo ni la SIDO na kwamba lina mgogoro mahakamani. Kandoro alitoa tathimini kuwa wafanyabiashara wapatao 1,206 ndio walioathirika na janga hilo ambapo kati yao ni wafanyabiashara 969 tu watakaobaki katika eneo hilo huku wengine 237 wakihamishiwa katika masoko mengine. Wakati Mkuu wa Mkoa akitoa taarifa hiyo, taarifa ya awali kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Beatha Swai siku ya tukio, ilisema kuwa jumla ya wafanyabiashara 1,350 walipoteza mali zao huku taarifa ya Mwenyekiti wa Soko hilo ikisema kuwa jumla ya vibanda 1,700 viliungua ambapo watu zaidi ya 2,000 wameathirika na janga hilo. |
Thursday, September 29, 2011
"NIMEACHWA, MIKOPO INANIFUNGA"- MUATHIRIKA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment